Ushahidi ndizi mahakamani

Kunguru alishika Kitabu cha Ukweli na kuapa kwamba atasema ukweli peke yake na kwamba hataongeza maneno ya kupotosha au kuwadanganya wasikilizaji.

Mzee Kobe alirudisha Kitabu cha Ukweli na kuanza kumhoji Kunguru. Kunguru alikuwa mmoja ya kati ya wale walioshuhudia ndizi ikiibiwa.

‘Kwanza jitambulishe. Utuambie majina yako kamili na kule unakoishi.’, Mzee Kobe akaanza.

‘Kwa majina mimi naitwa Kunguru wa Amosi. Mimi naishi Amosi pamoja na watoto wangu.’, Kunguru akajitambulisha.

‘Hebu tueleze mnamo tarehe kumi mwezi wa saba mchana ulikuwa na shughuli gani?’, Mzee Kobe akauliza.

‘Mimi nilikuwa nikielekea sokoni kununua mahindi.’, Kunguru akajibu.

‘Kutoka kule unakoishi hadi sokoni ni safari ndefu?’, Kobe akaendelea.

‘Ni safari ya kawaida na huwa inanichukua dakika kumi hivi.’, Kunguru akajibu.

‘Je, uliona jambo lisilo la kawaida? ‘, Kobe akauliza akiwa ameshika miwani yake.

‘Niliona Paka akiiba ndizi.’, Kunguru akajibu.

Mara hiyo kukawa na kelele kotini.

Rasto Paka alikuwa amepandishwa kizimbani kwa kosa la kumwibia ndizi na kumsababishia hasara Mbuzi na Kondoo ambao walikuwa wakila ndizi. Rasto Paka aliposomewa mashtaka na Hakimu Twiga Mkuu alikana.

‘Umewahi kuona paka akila ndizi?’, Paka akafoka.