Urafiki wa Chui waleta utata

chui
ngoma ya chui

‘Sitakwenda MJINI TENA!’, Paka akafoka akibubujikwa na machozi.

‘Kwa nini Paka?’, Teke Punda akauliza.

Hujamwona rafiki yangu chui?’, Paka akauliza Teke Punda.

‘Sijamwona kwa muda’, Teke Punda akajibu.

‘Sasa hivi amelazwa hospitalini kutokana na risasi alizopigwa wakati chui alipokabiliana na Binadamu.’, Paka akaendelea.

‘Alipigwa risasi na yungali hai. Chui ni jasiri.’,Teke punda akasema.

‘Wewe huelewi, chui alitaka kufanya urafiki na Binadamu, lakini hawakuelewana ndipo Binadamu kaamua kumfyatulia risasi.’,Paka akasema.

‘Hatari kwa lango! Nini kilimfanya chui afikirie kuwa rafiki wa Binadamu?’, Teke punda akauliza.

‘Pengine aliona afanye urafiki naye ndiposa aweze kumfanya kileo chake.’, Panya akachanga mawazo yake.

‘Akili yako panya ni duni sana. Wewe unafikiria jamii yetu ya paka ni kuwaza kileo kila dakika.’, Paka akamrudishia Panya.

‘Hebu tueleze vile mambo yalivyotendeka.’, Teke punda akamwomba Paka.

‘Chui alikuwa na wazo mzuri la kufanya urafiki na Binadamu ndiposa akaamua kuelekea mjini. Alifika mjini na alipojaribu kuanza kwa salaamu Binadamu alitoroka na kuita wenzake. Salaamu zake zilichukuliwa kama vitisho. Walimtupia mawe lakini chui aliwashinda kwa nguvu.’, Paka akasimulia.

‘Binadamu alitoroka na kurudi tena akiwa amejihami na mavazi ya kijeshi na kumfyatulia risasi moja baada ya nyingine. Chui alitoroka kuhepa hilo shambulizi.’, Paka akaendelea.

‘Zile zilikuwa risasi za usingizi. Sasa hivi angekuwa hayupo kama zingekuwa risasi asili. ’, Panya akachangia.

‘Baadaye Chui alianza kuyumbayumba kama mlevi na baadaye kuanguka tifu! Binadamu walimcheka alipoishiwa na nguvu. Chui sasa yuko hospitalini akipata matibabu. Hawezi kuwasiliana na yeyote amepoteza fahamu.’, Paka akasema.

‘Ha! Ha! Chui mlevi. Sasa ni wakati mzuri wa kuwasiliana naye nimpatie maono yangu.’, Panya akasema.

‘Binadamu anataka vipi?’, Teke punda akauliza kwa sauti.

‘Mimi simwelewi pia.’, Paka akasema.

‘Hujasikia kwamba Binadamu amezindua dawa ya kuwafanya mbu washibe.’, Panya akasema.

‘Mbona mbu pekee? Mimi pia ningependa niwe nimeshiba nyakati zote.’, Teke punda akasema.

‘Chui angesaidika na hiyo dawa. Hangefikiria kwenda kuzurura zurura mjini. Lakini mbona Binadamu kusaidia wadudu na kutuwacha sisi?’, Paka akaongeza.

Mbu humkosesha Binadamu usingizi. Akiwa ameshiba Binadamu atalala.’ , Panya akachanga mawazo yake.

‘Maisha mazuri hayo. Paka angepewa hiyo dawa atawacha kukusumbua tena au sivyo Panya?’, Teke punda akasema yake.

‘Hapo umenena Punda.’, Panya akarudisha.