Akipenda chongo huita kengeza

selfi

‘MADARAKA ni wapi?’ , tekepunda akauliza.

‘Kwa nini punda, unataka kuhama?’, Rasto akauliza kwa hamu.

‘Kabila alitumwa huko madarakani kufanya kazi ya umma. Sasa amekwama. Ameshindwa kuondoka madarakani.’, Tekepunda akaendelea.

‘Pengine shida ni nauli ya kulipa basi.’, Boflo akachanga mawazo yake.

‘Kabila ashindwe kulipa nauli? Hiyo ni aibu kubwa. Sifikiri shida ni nauli. Isitoshe madaraka ni hapa karibu.’,Tekepunda akaendelea na mawazo yake.

‘Basi pengine amezuiliwa.’,Boflo akasema.

‘Hataki kuondoka kwa sababu maisha ni mazuri kule madarakani. Hebu fikiria ukifanyia kazi umma unanona pia. Mwili unapata nafuu mara dufu!.’,Tekepunda akaendelea huku Rasto akicheka.

‘Sasa nimeelewa…unakula mali na uma!’,Boflo akawika.

‘Sikiza TUME YA UCHAGUZI itaamua yule atakaye kwenda madarakani Kabila akikubali kuondoka.’ Rasto akawaeleza.

‘Yani wakati Kabila atakaposhiba ndipo atakapoondoka madarakani.’,Boflo akaongeza akipapasa tumbo lake.

‘Kumaanisha kuwa mwingine akienda huko madarakani atakwama huko.’Tekepunda akaendelea.

‘..na hivyo ndivyo mambo yalivyo.’, Rasto akawaambia.

‘Kama ni hivyo hata mimi ningependa kuwa madarakani’, Boflo akasema.