Kulikuwa na kundi kubwa la nzige waliokuwa wakihamahama kutoka sehemu moja hadi nyingine, wakisababisha hofu kwa wakulima. Nzige hawa walikuwa maarufu kwa tabia yao ya kula kila kitu kinachokutana na meno yao makali.
Siku moja, walifika kwenye shamba kubwa lililopambwa na mahindi yaliyokomaa, mabichi na matamu. “Hii ndiyo shamba letu la neema!” nzige mmoja alitangaza kwa furaha. Wote waliingia shambani kwa kasi, wakaanza kula mahindi na hata matawi ya mimea.
Baada ya masaa kadhaa ya kushiba kupita kiasi, nzige walihisi mzigo wa kula kwao. Tumbo zao zilikuwa nzito, na hata kuruka ilionekana kuwa kazi ngumu. Kiongozi wao, nzige mkubwa mwenye maarifa ya safari, alisema, “Wenzangu, tunahitaji kuhama haraka. Habari zimeenea kwamba wakulima wamepanga kutupulizia dawa ili kutumaliza.”
Walijikusanya wote na kuelekea kwenye uwanja wa ndege wa karibu, wakiwa na matumaini ya kukodisha ndege ili kuwasaidia kuhama haraka. Walipofika, waliwasalimu rubani wa ndege kubwa, Bwana Korongo, na kusema kwa kiburi, “Tunataka kupanda ndege yako! Tuna haraka.”
Korongo, akiwa mwenye busara, aliwatathmini nzige kwa jicho la haraka. “Ninyi mmelewa tamaa,” alisema. “Mmejaa kupindukia. Hakuna ndege itakayoweza kubeba uzito wenu.”
Nzige hawakusikiliza. Walisisitiza, “Tutakulipa kwa dhahabu ya shamba hili tulilovamia.”
Korongo akatikisa kichwa, “Dhahabu haina maana kama nyinyi ni mzigo kwa ndege yangu. Jaribuni kupunguza uzito kwanza.”
Wakati mjadala ukiendelea, wakulima walifika kimyakimya wakiwa na pampu za dawa mikononi mwao. Walipulizia dawa ya sumu kwenye uwanja mzima wa ndege. Harufu kali ilienea kila mahali.
Nzige wakaanza kuhisi athari mara moja. Wengine walizirai pale pale, wakidondoka chini ya viti na meza za uwanja wa ndege. Wengine walijaribu kuruka juu, lakini uzito wa tumbo zao ukawa kikwazo. “Hatuwezi kuruka!” nzige mmoja alipiga kelele kwa hofu.
Kwa muda mfupi, uwanja mzima ulikuwa kimya. Nzige wote walikuwa wamelala, wakiwa hawana nguvu kutokana na sumu na mzigo wa mahindiĀ mjadala,waliokula.
Tangu siku hiyo, nzige waliojionea tukio hilo walijifunza somo kubwa. Walipokuwa wakisikia sauti ya ndege, walikimbia haraka, wakihofia kurudia hali ya zamani. Hadithi ya nzige na ndege ilienea kila mahali, ikiwa onyo kwa wanyama wote juu ya madhara ya tamaa na uvivu.