Mheshimiwa anacheza ngoma kitamaduni

mheshimiwa na kuku

Kulikuwa na mwanasiasa mmoja maarufu kwa jina Mheshimiwa Bosi, mtu wa kujigamba na kujionesha kuwa na uwezo mkubwa wa kushawishi watu. Katika kila kampeni, alitegemea mbinu moja kuu: kuwaga mahindi kwa kuku. Hapa, “kuku” walikuwa wananchi wa kawaida waliopapatika kwa ahadi na pesa ndogo ndogo, huku “mahindi” yakiwa ni zawadi kama pesa taslimu, mifuko ya unga, au ahadi tupu zisizokuwa na msingi.

Siku moja, akiwa katika kijiji cha Kijogoo ambako alikuwa na ufuasi mkubwa, Mheshimiwa Bosi alifika kwa mbwembwe akiwa na msafara wa magari ya kifahari. Alishuka kwenye gari lake aina ya V8 akiwa amevaa suti ya gharama na miwani ya giza. Alikaribishwa na nyimbo za kumsifu kutoka kwa vikundi vya vijana na wanawake walioahidiwa posho baada ya mkutano.

Baada ya hotuba yake ndefu iliyojaa ahadi nyingi, Mheshimiwa Bosi aliamua kugawa mahindi – si halisi, bali ahadi za kununua kura. Aliahidi mashine za kusaga nafaka, daraja jipya, na hata mwalimu wa ziada kwa shule ya kijiji. Kwa kila mtu aliyemkaribia, alitoa noti mpya za shilingi mia mbili na kuwasihi wapige kura kwa jina lake. Wanakijiji, kwa kawaida yao, walishangilia kwa shangwe.

Lakini, kijijini palikuwa na mzee mmoja mwerevu kwa jina Babu Kuku. Huyu mzee alikuwa na kuku wake wengi waliokuwa maarufu kwa ujeuri na maadili ya kutetea haki. Babu Kuku aliposikia Mheshimiwa Bosi akiahidi ahadi hewa, alikasirika. Alisema kwa sauti kubwa:

“Mheshimiwa, huwezi kuwadanganya watu kila msimu wa kura. Unatoa mahindi lakini unaturudia na mashoka ukishinda! Leo tutakufundisha somo.”

Mzee Kuku aliamuru kuku wake wote – weupe, wekundu, na hata mweusi wa kidume – kutoka bandani na kumvamia Mheshimiwa Bosi. Kwa mshangao, kuku walitii bila kusita. Walianza kumfukuza Mheshimiwa Bosi, huku wakipiga kelele na kumpapatikia.

Mheshimiwa Bosi, ambaye hakuwa na desturi ya kukimbia, alijikuta akiacha gari lake na kukimbia kwa miguu. Alipita vichochoro vya kijiji, akiruka mitaro na mabonde huku akiropokwa:

“Kwa nini mnifukuza wakati nimewagawia mahindi?!”

Lakini kuku walimfuata bila huruma. Alijaribu kujificha nyuma ya mnazi, lakini jogoo mmoja mkubwa alimkuta na kumkimbiza zaidi. Hatimaye, Mheshimiwa Bosi alipanda juu ya mti wa mwembe akitetemeka, huku kuku wakimzunguka chini wakitoa kelele za kishindo.

Wanakijiji walikusanyika na kucheka hadi machozi. Walipaza sauti:

“Mheshimiwa, kura yetu si ya mahindi! Tunataka maendeleo, si ahadi!”

Katika hali hiyo ya aibu, Mheshimiwa Bosi alilazimika kuita walinzi wake waje kumuokoa. Wakati walinzi walipofika, walimshusha kutoka juu ya mwembe na kumchukua kwa gari lake lililokuwa limejaa vumbi. Wanakijiji walimwambia kwa dhihaka:

“Rudi na maendeleo, si mahindi.”

Tangu siku hiyo, jina lake likabadilika kuwa Mheshimiwa Jogoo, na kila alipopita, watu walimwambia:

“Sisi si Kuku utudanganye kwa mahindi. Tunahitaji haki!”

Hivyo ndivyo jinamizi la kuku lilivyomfundisha Mheshimiwa Bosi kuwa si kila kura inanunuliwa – nyingine hutolewa kwa moyo wa dhati wa maendeleo