Samaki na flamingo walipenda sana kuogelea ziwani. Kwa sababu hii wakawa marafiki. Kila walipokutana katika ziwa majisafi flamingo alimpa samaki uhondo za kule alikokuwa na yale aliyoyaona. Samaki naye alimhadithia flamingo matukio ya kule ndani majini.
Wakati mwingine flamingo alimhadithia samaki kuhusu vyakula vitamu alivyokuwa akila milimani na ndio sababu alikuwa na afya nzuri. Alisema pia hewa safi aliyokuwa akipumua kule angani ilikuwa inasafisha mwili wake kutoka makali ya maji ya ziwa majisafi.
Samaki alisikia haya yote na alitamani sana kuona na kula vitamu lakini haingewezekana kwa sababu hakuwa na mabawa kama flamingo.
Siku moja flamingo akamwelezea samaki kuwa kuna karamu kubwa ilyokuwa imeandaliwa kule milimani na kwamba wote wamealikwa. Samaki akamwomba flamingo amletee vitamu ili aweze pia kuonja. Flamingo akakubali na siku iliyofuata akajiandaa na kuelekea milimani kwa karamu.
Akiwa angani akaona sufuria kubwa iliyokuwa na harufu nzuri ya chakula kitamu. ‘Duh’ , alisema flamingo ‘Sufuria kubwa jameni. Chakula imo ndani yake kitamu kinavutia. Mle ndani lazima nitaingia.’
Ghafla bin vu akashuka kutoka angani kwa kasi huku macho yakiwa yamelenga sufuria.
Asijue kwamba sufuria ilikuwa na supu moto flamingo akaingia ndani kwa miguu yake yote miwili kama kuogelea ndani ya maji. Alipiga mayowe na kutoka mbio huku akidondonkwa na machozi ya uchungu. Hadi sasa anapoingia majini mguu wake mmoja huinua kama kupima hali joto kabla ya kuingiza yote.